Watoa chanjo washambuliwa Pakistan

Haki miliki ya picha BBC World Service
Image caption Shambulio la bomu dhidi ya watoa chanjo ya polio, Pakistan

Watu wapatao 11 wameuawa katika shambulio la bomu dhidi ya watoa chanjo ya polio kaskazini magharibi mwa Pakistan.

Bomu lililokuwa limetegwa kando ya barabara lilifyatuka wakati msafara uliokuwa ukilindwa na polisi ukipita katika kijiji kimoja katika jimbo la Khyber Pakhtunkhwa karibu na mpaka na Afghanistan.

Shambulio hilo ni jipya kabisa miongoni mwa mashambulio yanayowalenga watoa huduma ya chanjo ya polio nchini Pakistan.

Hakuna kundi lililodai kuhusika na shambulio hilo, lakini kundi la Taliban limekuwa likipinga mipango ya utoaji wa chanjo ya polio, mipango ambayo wanaichukulia kama mbinu ya ujasusi wa kimataifa.

Taarifa za awali zilisema msafara huo ulishambuliwa na makombora mawili tofauti siku ya Jumamosi.

Milipuko hiyo imeripotiwa kufuatiwa na mapigano makali ya bunduki kati ya majeshi ya usalama na wanamgambo.

Maafisa wamethibitisha kuwa watu waliojeruhiwa katika shambulio hilo walikimbizwa katika hospitali ya karibu. Baadhi ya waliojeruhiwa wanasemekana kuwa katika hali mbaya.

Pakistan imeshuhudia vitendo vya ghasia kufanyiwa wafanyakazi wa afya, ambao wanamgambo wanawatuhumu pia kuwa sehemu ya njama za nchi za magharibi kupunguza idadi ya Waislam.

Zaidi ya watu 40 wanaohusishwa na mpango wa chanjo wameuawa nchini Pakistan tangu Desemba 2012.

Mwezi uliopita, watu wenye silaha wasiofahamika waliwaua kwa kuwapiga risasi wafanyakazi watatu wa kutoa chanjo ya polio, katika mji wa Karachi ulioko kusini mwa Pakistan, siku moja baada ya serikali kuanza zoezi la chanjo kwa nchi nzima.

Pakistan ni moja kati ya nchi tatu zinazokabiliwa na milipuko ya ugonjwa wa polio, duniani zikiwemo Nigeria na Afghanistan.

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani, WHO, Pakistan ilikuwa na wagonjwa 91 wa polio mwaka jana, wakiwa wameongezeka kutoka idadi ya wagonjwa 58 mwaka 2012.