Ukraine yajizatiti kijeshi

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Askari wa Urusi huko Crimea, nchini Ukraine

Ukraine imeagiza kuimarisha vikosi vyake katika kukabiliana na Urusi ambayo inaimarisha jeshi lake katika jimbo la Ukraine la Crimea.

Kaimu Rais wa Ukraine Olexander Turchynov ameagiza kufungwa kwa safari za anga la nchi hiyo kwa ndege zote zisizo za kiraia.

Rais wa Marekani Barack Obama ameeleza usambazaji wa majeshi ya Urusi katika jimbo hilo ni "kuingilia uhuru wa Ukraine".

Waziri mkuu mpya wa jimbo la Crimea lenye mamlaka ya kujiamulia mambo yake lenyewe, Sergiy Aksyonov, mwenye mwelekeo wa kuipendelea Urusi, amesema amemwomba Bwana Putin ili kuhakikisha usalama wa eneo hilo.

Hata hivyo serikali ya mpito ya Ukraine haimtambui Bwana Aksyonov na serikali yake ya Crimea.