Obama ataka wachunguzi kutumwa Ukraine

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Hali ya wasiwasi imekumba jimbo la Crimea.

Rais Obama ametangaza mapendekezo ambayo huenda yakatoa suluhu kwa mzozo wa Ukraine, ikiwemo kuwatuma wachunguzi wa kimataifa na kuanzishwa mazungumzo ya moja kwa moja kati ya Moscow na serikali mpya mjini Kiev.

Bwana Obama amejadili swala hilo kwa njia ya simu na chanzela wa Ujerumani, Angela Merkel.

Wachunguzi hao watalenga kulinda haki za watu wa kabila la Urusi waliopo katika jimbo la Crimea; na kwa upande wake Urusi itahitajika kuwaondoa wanajeshi wake katika jimbo hilo. Pendekezo hilo huenda likajadiliwa pembezoni mwa mkutano utakaofanyika nchini Ufaransa (Jumatano) ambao utawaleta pamoja wajumbe kutoka Marekani, Urusi na kwingineko kwa ajili ya kuijadili Lebanon.

Hapo awali waziri wa mashauri ya nchi za kigeni wa Marekani John Kerry, amelaani kile amekitaja kuwa kitendo cha uchukozi kutoka Urusi dhidi ya Ukraine. Wakati wa ziara yake mjini Kiev ambapo aliweka shada la maua kuwakumbuka waandamanaji waliouwawa mwezi uliopita, bwana Kerry ameshutumu Moscow kwa kutumia uongo na vitisho kuficha ukweli.

Mwandishi wa BBC Sarah Reinsford aliyepo mjini Kiev amesema kuwa wakati akiweka shada la maua katika maeneo walikouwawa mamia ya waandamanaji mjini humo, John Kerry alikaribishwa na umati wa watu waliokuwa wakiomba msaada wa marekani.

Na hilo ndilo lililomleta hapa; kutoa msaada wa hali na mali na pia wa kisiasa kwa serikali ya mpito ya Ukraine, na pia ahadi ya msaada wa kifedha na wa kiufundi kusaidia katika kuimarisha uchumi, amesema mwandishi wetu.

Haki miliki ya picha
Image caption Rais Putin.

Lakini zaidi ya yote bwana Kerry ameleta ujumbe kwa Moscow.

" Nadhani ni bayana kwamba Urusi imekuwa ikifanya bidii kubuni dhana ya kuiwezesha kutekeleza uvamizi zaidi. Urusi imezungumzia raia wachache wanaozungumza kirusi ambao wamezingirwa. Ukweli ni kwamba hawajazingirwa! Ukweli ni kwamba serikali mpya ya Ukraine imewajibika ipasavyo kwa kuhimiza utulivu na kujiepusha na uchokozi," amesema Bwana Kerry.

Haukuna ushahidi, amesisitiza, kwa madai ya urusi kwamba wanajeshi wake wanalinda raia wanaozungumza lugha ya kirusi nchini Ukraine akiishutumu moscow kwa kutumia uongo na vitisho kuficha ukweli.

Katika karne ya ishirini na moja, bwana Kerry ameonya, haiwezekani kuvamia taifa jingine na kisha kuamrisha matakwa yako yatekelezwe kwa kutumia mtutu wa bunduki. Na kisha akamhimiza rais Putin kuwaondoa wanajeshi wake katika jimbo la Crimea na kushughulikia malalamishi yake kupitia njia za kisheria na amani.

Lau sivyo, ameonya, kwamba Urusi itakabiliwa na vikwazo zaidi vya kiuchumi na kisiasa.