Rwanda yafukuza afisa wa Afrika Kusini

Jenerali Kayumba Nyamwasa

Waziri wa mashauri ya nchi za nje wa Rwanda amethibitisha kuwa serikali inawafukuza maafisa sita wa ubalozi wa Afrika Kusini, saa chache baada ya Afrika Kusini kuwataka raia watatu wa Rwanda kuondoka nchini humo.

Afrika Kusini ilichukua hatua hiyo baada ya nyumba ya mpinzani mmoja wa Rwanda anayeishi Afrika Kusini kushambiliwa siku ya Jumaane.

Jenerali Kayumba Nyamwasa, ambaye aliwahi kuwa mkuu wa majeshi nchini Rwanda, hakuwa nyumbani wakati wa shambulio hilo.

Nyumba yake iliharibiwa na komputa na baadhi ya nyaraka zilichukuliwa.

Jenerali Nyamwasa amenusurika na majaribio mawili mengine ya kumuuwa akiwa Afrika Kusini.

Tayari watu wanafanyiwa kesi ya kujaribu kumuuwa - wakiwemo Wanyarwanda watatu na Watanzania watatu.