Dawa ya HIV yaponya Saratani?

Haki miliki ya picha AP
Image caption Chanjo ya Saratani ya kizazi kwa wanawake

Dawa ambayo kwa kawaida hutumika kupunguza makali ya virusi vya UKIMWI imegunduliwa kuwa ina uwezo wa kutibu Saratani ya kizazi vikamilifu baada ya kipindi cha miezi mitatu katika utafiti uliofanywa Hospitali kuu ya Kenyatta nchini Kenya.

Matokeo ya utafiti huo ni hatua kubwa katika vita dhidi ya Saratani.

Dkt. Lynne na Dkt. Ian Hampson ambao ni watafiti kutoka chuo kikuu cha Manchester nchini Uingereza pamoja na Dkt. Orora Maranga wa hospitali kuu ya Kenyatta, waliijaribu dawa ya Lopinavir kwa wagonjwa 40 kwa kipindi cha majuma mawili.

Miezi mitatu baadaye zaidi ya asilmia 90 ya wagonjwa hao walipatikana kupona kutokana na ugonjwa huo wa Saratani.

Taarifa ya chuo kikuu cha Manchester ilisema kuwa kati ya wanawake 23 waliotambuliwa kuugua ugonjwa huo wenye makali zaidi, 19 waliweza kurudi katika hali yao ya afya ya kawaida na kwa wawili makali ya Saratani yalionekana kupungua.

Wanawake 17 wengine ambao pia waligunduliwa kuwa na ugonjwa huo ambao ulikuwa katika awamu ya kwanza, walipata buheri wa afya kama wenzao.

Ugunduzi wa utafiti huo ambao uliibua mjadala mkali katika chuo kikuu cha Manchester, iwapo ni ukweli, ni wa kushangaza na huenda ukawa ni miujiza katika matibabu ya Saratani ya kizazi miongoni mwa nchi zinazoendelea.

Pindi tu mtu anapogunduliwa kuwa na ugonjwa huo, mgonjwa anapaswa kumeza tembe moja ya dawa ya kupunguza makali ya UKIMWI mara mbili kila siku kwa muda wa majuma mawili.