Pistorius:Sehemu ya ushahidi kubanwa

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Pistorius amekana madai ya kumuua mpenzi wake kwa maksudi

Mwanariadha mlemavu wa Afrika Kusini Oscar Pistorius, ametapika mahakamani huku akisikia ushahidi kutoka kwa mtaalamu wa uchunguzi wa mauaji katika kesi dhidi ya Pistorius.

Mtaalamu huyo ametoa ushahidi kuhusu majeraha aliyoyapata marehemu mpenzi wa Oscar Reeva Steenkamp baada ya Pistorius kumpiga risasi na kumuua.

Gert Saayman aliambia mahakama kuwa Steenkamp alipigwa risasi mguuni, kwenye paja , kichwani na mkononi.

Mashahidi wa upande wa mashitaka katika kesi ya mauaji dhidi ya Oscar Pistorius wanaendelea kutoa ushahidi zadi dhidi ya mwanariadha huyo katika wiki ya pili ya kusikilizwa kwa kesi hiyo.

Upande wa mashitaka unanuia kuthibitisha kuwa bwana Pistorius alimpiga risasi maksudi aliyekuwa mpenzi wake Reeva Steenkamp mwaka jana wakati wawili hao walipokuwa wanagombana.

Pistorius amekanusha madai hayo akisema kua alimpiga risasi Reeva kwa bahati mbaya akidhani alikuwa jambazi aliyekuwa amevamia nyumba yao.

Wakati huohuo jaji anayesikiliza kesi hiyo amepiga marufuku kupeperusha kesi dhidi ya Oscar moja kwa moja kutoka mahakamani wakati ambapo picha za mauaji ya Reeva zitakapoonyeshwa.

Pistorius alitapika mahakamani aliposikia ushahidi kuhusu mauaji ya Reeva na kuona picha hizo.

Bwana Saayman alimshawishi jaji kutoruhusu kuonyeshwa kwa picha hizo akisema kuwa zinaonyesha majeruhi mabaya aliyoyapata Reeva na kwamba ni lazima mahakama iweze kumsitiri marehemu.

Jaji huyo pia alipiga marufuku mjadala wowote kuhusu picha hizo kwenye Twitter.