US kuzuia dhuluma za ngono jeshini

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Jeshi la Marekani kazini

Baraza la Senate la Marekani limeidhinisha kwa kauli moja mabadiliko ya hatua zinazopaswa kuchukuliwa kuhusiana na unyanyasaji wa kimapenzi katika jeshi.

Ushahidi umeimarika kuhusu visa vya unyanyasaji wa kimapenzi katika jeshi na wito umetolewa na makundi mbalimbali kuwa sheria mpya zibuniwe kukabiliana na dhuluma hiyo

Tatizo la ubakaji na makosa mengine ya ngono katika jeshi limeongezeka sana hivi kwamba makao makuu ya jeshi, Pentagon, yamefananisha matukio hayo kama saratani.

Mabadiliko yaliyoidhinishwa na Baraza la Senet yananuia kuimarisha jinsi kesi hizi zinavyoshughulikiwa katika Mahakama ya jeshi. Hata hivyo mabadiliko hayo lazima yaidhinishwe na Bunge la waakilishi.

Mojawapo wa hatua hizi ni kuondoa kinga ya sasa iliyopo ambapo mwanajeshi aliyebaka anaweza kudai kuwa yeye amefanya kazi yake ya kijeshi kistaarabu, na kwa hivyo anapaswa kuhurumiwa hata akipatikana na hatia.

Mabadiliko hayo yanakusudiwa kutumiwa katika kuhakikisha kuwa jeshi linawajibika.

Hata hivyo hatua hizo zimeepusha kuwatimua kazini makamanda ambao wanasimamia vitengo ambako makosa hayo yanatokea.