UN yaonya kuhusu mapigano Darfur

Haki miliki ya picha AFP
Image caption UN imetahadharisha dhidi ya kuzuka upya vita Darfur

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban-Ki-moon, ameelezea wasiwasi kuhusu kuzuka upya kwa vita katika jimbo la Darfur nchini Sudan.

Maelfu ya watu wamefariki katika vita vya miaka 11 katika jimbo hilo.

Katika taarifa yake Bwana Ban amezitaka pande zote kwenye mgogoro huo kusitisha vita mara moja.

Vita katika jimbo la Darfur, vimekuwa vikiendelea licha ya kuwepo wanajeshi 19,000 wa muungano wa Afrika chini ya kikosi kinachojulikana kama UNAMID.

Katika wiki moja iliyopita, wanajeshi wa UNAMID walisema kuwa walishuhudia uporaji na uharibifu katika mji wa Saraf Omra, mbao uko Mashariki mwa El-Geneina, mji mkuu wa jimbo la Darfur Magharibi.

Vita kati ya jamii za waarabu vimesababisha maelfu kutoroka makwao na kutafuta hifadhi karibu na kambi za jeshi la UNAMID.

Waliungana na watu wengine zaidi ya 40,000 walioachwa bila makao kufuatia vita vilivyozuka katika majimbo ya Darfur Kusini na Kaskazini.

Wachunguzi kadhaa wanasema kuwa ghasia ni mbaya kama ilivyokuwa mwaka 2003, wakati mgogoro huo ulipoanza.

Nyingi ya ghasia zilikuwa kati ya jamii za waarabu ingawa pia zilihusisha waasi walio katika eneo hilo ambao wamekuwa wakilaumu serikali na wanajeshi kwa kuzuka upya kwa ghasia hizo.

Wakati huohuo, kiongozi wa waarabu anayelaumiwa kusababisha vita, Musa Hilal, hivi karibuni alijiondoa serikalini na kutishia vita.

Watu milioni mbili wamepoteza makao yao katika jimbo la Darfur, tangu kuanza vita dhidi ya serikali mwaka 2003 baada ya kuituhumu kwa ubaguzi.