Damu nyumbani kwa Pistorius

Haki miliki ya picha
Image caption Polisi akitoa ushahidi katika kesi inayomkabili Oscar Pistorius

Polisi wameelezea mahakama kuwa waliona damu kwenye ghorofa ya nyumba alimokuwa anaishi Oscar Postorius siku ambapo mpenzi wake aliuawa.

Kanali Schoombie van Rensburg ameambia mahakama katika kesi inayoendelea dhidi ya Pistorius kuwa alimpata mwanariadha huyo katika hali ya kufadhaika punde baada ya mauaji ya Reeva Steenkamp.

Awali wataalamu wa uchunguzi wa mauaji walitetea polisi kuhusu walivyokusanya ushahidi wao.

Bwana Pistorius amekanusha madai ya kumuua mpenzi wake akisema kuwa alimpiga risasi akidhani alikuwa mwizi ndani ya nyumba yake tarehe 14 mwezi Februari mwaka 2013.

Upande wa mashitaka ulisema kuwa alijaribu kuugonga mlango wa bafu na kisha kufyatua risasi.

Kanali Van Rensburg, aliyekuwa mkuu wa uchunguzi katika tukio la mauaji, alisema kuwa alitoa amri mara moja ya eneo hilo kuzibwa ili uchunguzi uendelee.

Wakili wa upande wa utetezi, Barry Roux amesema kuwa ushahidi kutoka katika eneo la mauaji ulipotea.

Van Rensburg alisema aliona damu kutoka ghorofani ndani ya nyumba ya Oscar pamoja na chembe chembe za damu kwenye viti sebuleni.

Mahakama ilionyeshwa picha za eneo la mauaji ambazo zilionyesha damu kwenye kuta za ghorofa. Kesi hiyo itaendelea hapo kesho Ijumaa.