Rwanda yahusishwa na uvamizi A. Kusini

Image caption Kayumba Nyamwasa

Afrika Kusini imewatuhumu wanadiplomasia watatu wa Rwanda waliofurushwa kutoka nchini humo kwa kuhusika na mauaji na njama ya mauaji dhidi ya wapinzani wa serikali ya Rwanda wanaoishi Afrika Kusini.

Waziri wa sheria wa Afrika Kusini, Jeff Radebe amesema kuwa ana ushahidi wa kutosha unaowahusisha watatu hao na vitendo vyinavyokiuka sheria.

Wanadiplomasia hao, walifurushwa siku ya Ijumaa baada ya kutokea uvamizi nyumbani kwa Generali Kayumba Nyamwasa aliyekuwa wakati mmoja mwandani wa Rais Kagame, mjini Johannesburg.

Rwanda ambayo nayo iliwafurushwa wanadiplomasia sita wa Afrika Kusini kutoka mjini Kigali, imekanusha madai ya kuhusika na njama hiyo.

Msemaji wa Bwana Radebe, Mthunzi Mhaga, aliambia BBC kuwa uchunguzi ulibaini kuwa watatu hao walihusika na uvamizi huo na mashambulizi mengine dhidi ya watu wanaoonekana kuwa wapinzani wa serikali ya Rwanda wanaoishi nchini Afrika Kusini.

Watu waliokuwa wamejihami, walivamia nyumba ya Luteni Generali Nyamwasa, mkuu wa zamani wa majeshi ya Rwanda wiki jana lakini hakuwepo nyumbani wakati wa uvamizi huo.

Wavamizi hao walifanya msako ndani ya nyumba hiyo na kuondoka wakiwa wamebeba Komputa na stakabadhi kadhaa.

Generali Nyamwasa ameponea majaribio mawili ya kumuua ikiwemo kupigwa risasi mjini Johannesburg mwaka 2010 baada ya kutoroka Rwanda.

Alitafuta hifadhi nchini Afrika Kusini baada ya uhusiano wake na Kagame kuvunjika.

Januari mwaka huu mwili wa aliyekuwa jasusi mkuu wa Rwanda, Patrick Karegeya, ulipatikana ndani ya hoteli moja mjini Johannesburg akiwa na alama za kunyongwa.

Maafisa wa zamani wa serikali ya Rwanda waliokimbilia usalama wao katika nchi za Magharibi ikiwemo Uingereza na Marekani wanasema kuwa maafisa wa usalama wa serikali wametishia kuwaua.

Muda mfupi baada ya kifo cha Karegeya Rais Kagame alionya kuwa wale ambao wanasaliti nchi hiyo watakiona cha mtema kuni.

Afrika Kusini ilikuwa wakati mmoja mshirika mkubwa wa Afrika Kusini na hata kununua silaha kutoka kwake, lakini uhusiano kati ya nchi hizo umeendelea kuzorota kila kukicha kufuatia mashambulizi dhidi ya waliokuwa maafisa wa Rwanda waliokimbilia nchini humo.