Kenya:Kuzuia usafiri wa usiku sio haki

Image caption Moja ya Basi la usafiri wa usiku liliohusika katika ajali mbaya ya barabarani

Agizo la serikali ya Kenya kuzuia usafiri wa usiku wa magari ya abiria linakiuka uhuru wa wananchi wa nchi hiyo kusafiri.

Hii ni kwa mujibu wa uamuzi wa mahakama kuu mjini Nairobi iliyotoa siku sitini kwa serikali ya Kenya kubuni sheria bora na mikakati mizuri ya kuboresha usafiri wa barabarani nyakati za usiku.

La sivyo mahakama itachukua hatua nyinginezo.

Jaji aliyetoa uamuzi huo George Odunga alisema kuwa serikali inaingilia haki za wasafiri kwa kuwamuuru kutosafiri usiku katika juhudi zake za kupunguza ajali za barabarani.

Serikali ya Kenya ilipiga marufuku usafiri wa usiku kwa kutumia magari na mabasi ya umma mwezi Disemba ili kupunguza ajali za barabarani ambazo zilikuwa zinaongezeka kila kukicha.

Kwa hilo jaji alisema kuwa serikali inapaswa kubuni mikakati na sheria bora za kukabiliana na ajali za barabarani na uendeshwaji mbaya wa magari ya abiria.

Kadhalika alisema kuwa jukumu la kuhakikisha usalama barabani halipwasi kuachiwa wamiliki wa magari ya abiria.

Pia ameitaka wizara ya usafiri na uchukuzi kushauriana na wadau katika sekta ya usafiri waliokwenda mahakamani kupinga agizo la serikali kuzuia usafiri wa mabasi ya umma usiku.

Mji mkuu Nairobi ni kitovu cha shughuli nyingi za mabasi ya usafiri ambayo hubeba abiria wanaosafiri kwenda katika nchi tofauti za kanda ya Afrika Mashariki.