Mkanyagano waleta maafa Nigeria

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Polisi nchini Nigeria

Watu kadhaa wameuwawa na wengine wengi kujeruhiwa baada ya vurumai kutokea pale walipokuwa wakihudhuria zoezi la serikali la kuwaajiri watu kazi katika miji kadhaa Nchini Nigeria.

Maelfu ya watu waliokuwa na hamu kubwa ya kupata ajira, walijitokeza kwa wingi katika zoezi hilo kote Nchini humo. Walikuwa wamejitokeza katika ofisi za wizara ya uhamiaji.

Walioshuhudia wamesema kuwa karibu watu saba wamekufa pale umati uliposukumana katika lango kuu la uwanja wa kitaifa wa michezo mjini Abuja.

Wengine walipoteza maisha yao katika uwanja wa michezo wa Port Harcourt na uwanja wa shule katika mji wa Minna.

Tatizo la ajira kwa vijana ni kubwa mno Nchini Nigeria huku zaidi ya robo tatu ya vijana walio na chini ya umri wa miaka 25 wakiwa bila kazi.

Maelfu ya watu walijitokeza kufanya mtihani wa ajira - inaarifiwa mkanyagano ulitokea walipojaribu kufika katikati ya uwanja.