Malaysia yaomba data na rada ya ndege

Haki miliki ya picha AP

Serikali ya Malaysia imeomba kupewa radar zaidi pamoja na data ya satelite kutoka kwa mataifa mengi huku ikijitahidi kutafuta eneo la ndege ya kampuni ya Malaysia Airline iliopotea zaidi ya wiki moja iliopita.

Waziri wa uchukuzi nchini Malaysia Hishamuddin Hussein amesema kuwa takriban mataifa 25 yanashiriki katika kuitafuta ndege hiyo.

Aidha ameyashukuru mataifa hayo na kusema kuwa kiwango cha ushirikiano wao hakina kifani.

Kwa siku ya pili mfululizo maafisa wa polisi wamezuru katika nyumba ya nahodha mkuu Zharie Shah huku uchunguzi ukiendelea kuwaangazia abiria wote waliokuwa ndani ya ndege hiyo.

Naye ndugu mmoja ya mwathiriwa wa ndege hiyo amesema kuwa hatakwenda nyumbani hadi pale atakapopata majibu kamili kuhusiana na ndege hiyo.

Kwa sasa Malaysia inaangazia njia mbili ambazo huenda ndege hiyo ilielekea, nazo ni ukanda wa kazkazini na ule wa kusini.