Ufaransa yazongwa na hewa chafu

Haki miliki ya picha AFP

Serikali ya Ufaransa imezindua mfumo wa kuendesha magari kwa siku maalum mjini Paris, kama njia ya kujaribu kupunguza uchafuzi mkubwa wa hewa.

Kuanzia Jumatatu, madereva watatumia magari yao mara moja moja huku siku zingine wakitembea kwa miguu katika mji mkuu Paris.

Hii ni mara ya pili tangu mwaka 1997 kwa hatua hiyo kuongezwa nguvu.

Serikali iliafikia hilo katika tangazo lake la siku ya Jumamosi baada ya kiwango cha uchafuzi wa hewa kuzidi kwa siku tano za wiki mfululizo hasa katika mji wa Paris na viunga vyake.

Hali ya ukungu unaotanda kote Paris ni kutokana na hali ya baridi kali usiku na mchana jambo linalozuia hewa kuchanganyika vyema.

Mnamo siku ya Ijumaa serikali ilitoa usafiri bila malipo kwa wananchi ili kuwashashwishi kuacha kutumia magari yao. Hali hiyo itaendelea siku ya Jumatatu.

Wanasayansi wanasema kuwa uchafuzi wa mazingira mjini Paris umekuwa mbaya sana hata kuliko mji wa Beijing wenye mazingira chafu zaidi ya hewa duniani.

Mnamo siku ya Ijumaa, kiwango cha uchafuzi wa mazingira kilikuwa kikubwa zaidi kuwahi kushuhudiwa.

Serikali itatathmini viwango vya uchafuzi siku ya Jumatatu na kuona ikiwa itaongeza muda wa agizo hilo au la.