Waathiriwa wanyimwa matibabu Burkina Faso

Image caption Hospitali iliyokamilika kujengwa ya 'Pleasure Hospital' haitapata kutumia

Hospitali ya kwanza kuwahi kujengwa kwa ajili ya kuwasaidia wanawake waathiriwa wa ukeketaji nchini Burkina Faso imekuwa ikizua utata kwa muda sasa.

Hospitali hiyo maarufu kama 'Pleasure Hospital ' ilitarajiwa kufungua milango yake kwa waathiriwa, mapema mwezi huu lakini sasa serikali inasema kuwa hospitali hiyo haitafunguliwa kwa sababu ya changamoto za leseni.

Shirika lisilo la kiserikali la Marekani Clitoraid,lililoijenga hospitali hiyo na ambalo, kazi yake ni kuwarejeshea hisia wanawake waliokeketwa , linasema kuwa serikali ilikataa kuidhinisha kufunguliwa kwa hospitali hiyo kutokana na shinikizo za kanisa katoliki.

Wasimamizi wa hospitali hiyo walinuia kuleta madaktari wa kuwatibu wanawake walioharibikiwa sehemu zao nyeti wakati wakifanyiwa ukeketaji.

Katika matibabu ambayo yangetolewa kwa mamia ya wanawake katika hospitali hiyo, ni kupasua kovu lililoachwa kutokana na ukeketaji na kisha kurekebisha sehemu hiyo kwa kurejesha hisia kwa mwanamke, wengi ambao wanasema kuwa wanahisi uchungu wakati wa tendo la ndoa.

Hospitali hiyo ilianza kujengwa mwaka 2011.

Image caption Baadhi ya wanawake waathiriwa wa ukeketaji

Lakini wizara ya afya nchini humo imesema kuwa haitaruhusu ifunguliwe kwa sababu wasimamizi hawakuwa na idhini tangu mwanzoni kuijenga.

Kikundi cha madaktari wamarekani waliowasili kufanya upasuaji waliwatibu tu wanawake wahache kwa kutumia chumba walichopewa na daktari mmoja raia wa nchi hiyo. Lakini sasa wamepokonywa leseni zao za kuendesha upasuaji huo. Hawana budi ila kurejea makwao.

Ukeketaji unawaathiri zaidi ya wanawake na wasichana milioni 140, utamaduni huo ukikita mizizi zaidi Afrika ya kati, Mashariki ya kati na Asia.

Mangariba hutumia nyembe, visu na vigae vya glasi na vifaa vingine hatari kuwakeketa wanawake katika sehemu nyingi za Afrika. Tatizo hili pia linawaandama wanawake wanaoishi Ulaha hasa Uingereza.

Waathiriwa huvuja damu nyingi na kupata madhara mengine ya afya ya uzazi na pia kuhisi uchungu wakati wa kitendo cha ndoa.