Apokezwa jeneza lenye mzoga wa Paka

Image caption Familia ya Bwana Oganda inasema kuwa sio mara ya kwanza kwa kisa kama hiki kuikumba

Familia ya afisaa mmoja wa Elimu nchini Kenya imepigwa na butwaa baada ya kupata jeneza dogo likiwa limewekwa kwenye mlango wao mjini Kisumu Magharibi mwa Kenya.

Kwa mujibu wa taarifa ya gazeti la Taifa Leo, familia ya Afisaa huyo Elias Oganda, mwenye umri wa miaka 56, ilipata jeneza hilo dogo likiwa na mzoga wa Paka nje ya mlango wao na sasa inaishi kwa hofu kubwa.

Afisaa huyo anayefanya kazi katika wizara ya elimu, alisema kuwa hii ni mara ya nne katika miezi sita kupata jeneza kama hilo nyumbani kwake.

Polisi walifungua jeneza hilo na kupata mzoga wa Paka ndani yake. Walishuku kuwa Paka huyo alinyongwa na kuwekwa ndani ya jeneza hilo kwani hapakuwa na dalili yoyote ya damu.

Image caption Visa vingi kuhusu Paka bila shaka huwa ni vya kuogofya

Afisaa mkuu wa polisi katika eneo hilo amesema kuwa hili sio tukio la kwanza kushuhudiwa katika eneo hilo.

Bwana Oganda naye alisema kuwa jeneza hilo liligunduliwa na mkewe Joyce Oganda, mwenye umri wa miaka 50, usiku wa manane alipotoka nje kujisaidia.

''Nia ya mtu aliyefanya kitendo hicho haijulikani, mimi sijawahi kuhusika na mzozo wa ardhi'' alisema bwana Oganda aliyeongeza kuwa familia yake haijwahi kupata utulivu kwa mwaka mmoja uliopita kwani amekuwa akifanyiwa uchawi mara kwa mara.''

''Hii ni ardhi ya babangu na sielewi kwa nini watu wanataka kunitishia maisha kwa kutumia uchawi.''

Wakazi walikita kambi katika nyumba ya bwana Oganda kushuhudia mchawi aliyeletwa katika nyumba hiyo kutoka Sirare mpakani mwa Kenya na Tanzania kujaribu kujua ni nani aliyehusika na kitendo hicho.