Radi yaandama nchi maskini?

Image caption Nchini Brazil Radi zinaongezeka wakati majeruhi nao pia wakiongezeka

Radi inasemekana kuwaua na kuwajeruhi watu wengi ambao idadi yao inaongezeka kila uchao katika nchi zinazostawi. Hii ni kwa mujibu wa wataalam wa maswala ya hali ya anga.

Idadi ya waathiriwa huenda ikawa kubwa kuliko ile ya waathiriwa wa mikasa mingine inayotokana na hali mbaya ya hewa kama vile mafuriko na ukame.

"Kumekuwa na ongezeko la radi kupiga kila uchao, ikilinganishwa na siku za hapo nyuma.,” anasema Michael Nkalubo ambaye ni Kamishina wa idara ya hali ya hewa nchini Uganda. Nchi ambayo radi hupiga kila mara.

"Siwezi sema kuwa kuna utafiti maalum ambao umefanywa kuhusu swala hili, ila nasema haya kulingana tu na mtazamo wangu.

Ni jambo linalokithiri na nadhani ni kwa sababu ya mabadiliko ya hali ya anga, na tunahitaji kuchunguza iwapo ukataji mwingi wa miti, bila ya kupanda mengine unachangia pia,”alisema.

Afrika Kusini ni nchi nyingine ya Bara la Afrika ambapo vifo na majeraha yanayotokana na radi kupiga vinaongezeka. Maafisa wanasema.

Kusini Mashariki mwa Bara Asia, wataalam pia wanaamini kuwa visa vya radi kupiga na kuwajeruhi watu vinaongezeka kila uchao.

"Ni shida inayokuwa mbaya kila siku,” alisema Hartono Zainal Abidin, ambaye ni mtaalam wa maswala ya kinga dhidi ya radi nchini Malaysia.

Image caption Baadhi ya wataalamu wanasema kuwa hali ya mazingira ndio inachochea ongezeko la radi

Wataalam wa maswala ya hali ya hewa Kusini mwa Asia pia wanasema wameshuhudia kuongezeka kwa radi kupiga barani humo

"Mtazamo wangu ni kuwa, miaka michache iliyopita tumeshuhudia ongezeko la radi kupiga,” alisema Shamsuddin Ahmed, ambaye ni naibu mkurugenzi wa idara ya hali ya hewa ya Bangladesh

Mwanasayansi, Osmar Pinto Junior wa Shule ya kitaifa ya elimu ya maswala ya anga nchini Brazil, alisema kumekuwa na visa vya radi kupiga na kuwajeruhi watu nchini humo na pia katika maeneo mengine ya Latin Amerika.

Wataalam wa hali ya hewa kutoka nchi zinazostawi wanasema visa na athari zinazotokana na radi kupiga haviripotiwi sana kwani hufanyika katika maeneo yaliyoko mbali, hivyo basi kufanya kuweka rekodi kuwa kugumu.

Je ni kwa sababu ya joto jingi?

Wanasayansi wengine wanaamini kuwa, iwapo hali ya joto duniani na mingurumo itazidi kuongezeka, ndivyo pia visa vya radi kupiga vitaongezeka.

Idara ya kimataifa inayoangazia maswala ya mabadiliko ya hali ya anga, imesema: “Inatarajiwa kuwa visa vya radi kupiga vitaongezeka iwapo hali ya joto duniani pia itaongezeka.

Japo, kuna utafiti wa hali ya anga kabla mwaka 2030 ambao unasema kuwa visa vya radi kupiga, havitaongezeka bali vitasonga kutoka maeneo yaliyo mbali na ikweta hadi maeneo yaliyo karibu na ikweta.”

Wataalam wanakadiria kuwa kuna zaidi ya visa mia moja vya radi kupiga maeneo tofauti duniani kila sekunde, na zaidi ya 70% ya visa hivyo, vinafanyika katika maeneo ya wataalam yaliyo na joto jingi.

Nchi zinazostawi?

Professa Price alisema: "Nchi ambazo zingali zinakuwa ndizo zenye visa vingi vya radi kupiga-maeneo kama taifa Jamhuri ya Afrika ya Kati, Jamhuri ya Demokrasia Ya Congo, maeneo ya Amazon, Amerika Kusini, visiwa vya Indonesia, Borneo na Kusini Mashariki mwa Asia.

Image caption Wataalamu wanakinzana ikiwa mazingira yanasababisha kuongezeka kwa radi

Mtaalam wa hali ya hewa, Ron Holle, ambaye anafanya kazi na kampuni ya Finland ya Vaisala inayotengeneza vifaa vya kupima hali ya hewa, pia alisema kuwa Bara Afrika lina visa vingi vya radi kupiga.

"Katika miaka 10 iliyopita , tumegundua kuwa visa vya makali ya radi kupiga nchini Malawai, Swazilnad, Zimbabwe na maeneo mengine ya Afrika Kusini ni sawa tu na vile vya Marekani miaka 100 iliyopita.”

"Huenda imesababishwa na idadi ya watu, na hali ya maisha.”

Professa Price alikubali kuwa kuongezeka kwa idadi ya watu inachangia pakubwa visa vya radi kupiga.

Ila, si wanasayansi wote wanaokubaliana na hilo.

"Sijaona takwimu mahsusi zinazoonyesha kuwa kuongezeka kwa idadi ya watu duniani kumechochea visa vya radi kupiga,” anasema Professa, Robert H Holzworth, wa Chuo Kikuu cha Washington.

Wataalam wanasema kuwa Sayansi ya radi ingali ngumu kueleweka. Aidha wanasema kuwa tofauti ya maoni na mitazamo ya viongozi wa kisiasa na waundaji sera haijasadia kupata suluhu mahsusi kwa jambo hili.