Kiongozi wa upinzani aachiliwa Burundi

Image caption Frederic Bamvuginyumvira alichiliwa kwa dhamana ili aweze kupokea matibabu

Mahakama nchini Burundi imemwachilia kwa dhamana kiongozi mmoja mkuu wa upinzani aliyekabiliwa na kashfa za ngono pamoja na ulaji rushwa.

Wafuasi wake wanasema kuwa mashitaka hayo yalikuwa njama ya serikali kumzuia kushiriki uchaguzi mkuu kugombea urais dhidi ya Rais wa sasa Pierre Nkurunziza.

Frederic Bamvuginyumvira, makamu wa zamani wa Rais na kiongozi wa chama cha Front for Democracy (frodebu), alikamatwa mwezi Disemba akiwa ''katika kitendo cha ngono katika danguro,'' alisema afisaa mmoja wa mahakama.

Bwana Bamvuginyumvira alinyimwa dhamana mwezi Disemba lakini hapo jana mahakama ikatoa amri hiyo kutokana na hali yake mbaya ya kiafya.

Mahakama ilisema kuwa anaweza kuachiliwa aweze kupata matibabu ya shinikizo la damu.

Wakili wake Fabien Segatwa, alisema kuwa ''mahakama ya kupambana na ufisadi, imeamuru aachiliwe kwa dhamana na dola 600. Bwana Bamvuginyumvira hana sababu ya kuwa mahakamani kwani hana makosa yoyote. ''

Bamvuginyumvira, kiongozi anayeheshimika sana nchini Burundi, alisifika sana kwa kuwa mkali katika kupambana na rushwa na alikuwa makamu wa Rais kati ya mwaka 1998 hadi 2001. Kadhalika anaonekama kama mwanasiasa mwenye uwezo wa kumenyana na Rais katika uchaguzi mkuu.

Wengi wanaona kama huenda akajitosa kwenye uchaguzi mkuu mwaka 2015.