Malaysia:Msako waingia wiki ya 3

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Juhudi za kuisaka ndege ya Malaysia bado zinaendelea

Ndege na meli za Australia zimeanza siku ya tatu kufanya msako katika bahari hindi ambako waziri mkuu wa nchi hiyo alisema mabaki yanayoaminika kuwa ya ndege ya Malaysia iliyopotea wiki mbili zilizopita yalionekana.

Mawimbi ya bahari yametulia na hali ya anga inasemekana kuwa nzuri zaidi kuliko siku mbili zilizopita.

Ndege sita zinatafuta kwa udi na uvumba kilichosemekana kuwa mabaki ya ndege hiyo yaliyonaswa na mtambo wa Satelite wa Australia, yakiwa yanaelea baharini , umbali wa kilomita elfu mbili na miatano Kusini Magharibi mwa mji wa Perth.

Ndege hiyo, ilitoweka wiki mbili zilizopita, ikiwa na abiria miambili na arobaini. Ndege zaidi kutoka China na Japan zinatarajiwa kujiunga na msako huo katika siku chache zijazo.

Msako huo umeingia wiki yake ya tatu , lakini hakuna kilichopatikana kuongeza matumaini kuwa ndege iko salama.

Ndege hiyo MH370, ilipoteza mawasiliano ilipokuwa njiani kutoka Kuala Lumpur kuelekea Beijing tarehe 8 mwezi Machi.

Maafisa nchini Malaysia wanashuku kwamba mawasiliano ya ndege hiyo yalikatizwa kwa maksudi.