Papa Francis awaasa 'Mafia' kutubu

Haki miliki ya picha AP
Image caption Mkuu wa Mafia Italia Salvatore Riina

Kiongozi wa kanisa katoliki duniani Papa Francis amewaonya wanachama wa genge la Mafia kwamba watakwenda motoni iwapo hawatatubu dhambi zao.

Akizungumza katika sherehe ya maombi ya ndugu na jamaa za waathiriwa wa genge hilo waliouawa nchini Italia,Papa Francis amesema kuwa wanachama wa kundi hilo hawawezi kutumia fedha wanazopata kwenda peponi.

Wakati wa ibada hiyo majina ya watu 800 waliouawa na wanachama wa genge hilo yalisomwa.

Waandishi wanasema kuwa lengo la ibada hiyo ilikuwa kuonyesha kwamba kanisa katoliki linapinga uhalifu mbali na kujitenga na wakuu wa genge hilo wanaodai kuwa wafuasi wakubwa wa kanisa hilo.