Hewa chafu inaua mamilioni duniani

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Idadi kubwa ya watu waliofariki kutokana na hewa chafu walitoka katika nchi zinazostawi

Watu milioni saba walifariki mwaka 2012 kutokana na hewa chafu. Hii ni kwa mujibu wa shirika la afya duniani .

Ripoti ya shirika hilo inasema kuwa kuna uhusiano mkubwa kati ya hewa chafu na maradhi ya moyo, tatizo la kupumua na ugonjwa wa Saratani.

Kifo kimoja kati ya vinane duniani kilitokana na hewa chafu , na kuifanya hali hiyo kuwa moja ya hatari ya mazingira chafu afya ya binadamu.

Tarkriban watu milioni sita waliofariki dunia walikuwa Asia ya Mashariki na katika eneo la Pacific.

Shirika hilo limesema kuwa takriban watu milioni 3.3 walifariki kutokana na hewa chafu katika nyumba zao kwa kutumia mkaa kukipikia na wengine milioni 2.6 walifariki kutokana na hewa chafu nje ya nyumba zao , hasa katika nchi zinazostawi.

Afisaa mmoja mkuu wa shirika hilo, Daktari Maria Neira, amesema kuwa, hewa chafu ina hatari kubwa kwa afya ya watu kuliko ilivyodhaniwa hasa kwa kusababisha maradhi ya Moyo na Kiharusi.

Ripoti hii inaonyesha umuhimu wa kushirikiana katika kuhakikisha kuwepo kwa hewa safi.

Shirika hilo limesema kuwa kupunguzwa kwa viwango vya hewa chafu kunaweza kuokoa maisha ya watu.

Kadhalika shirika hilo limesema: "usafi wa hewa tunayopumua unazuia maradhi ya kuambukizana na pia kuondoa hatari kwa watoto, wazee na wanawake.''