Kesi ya Pistorius yaahirishwa Aprili 7

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Mahakama yaahirisha kusikizwa kwa kesi ya Oscar Pistorius

Kesi ya mwanariadha wa Afrika kusini Oscar Pistorius imeahirishwa baada ya mmoja wa mahakimu kuugua.

Mshindi huyo wa nishani ya dhahabu ya olimpiki , tayari alikuwa amewasili mahakamani ,ambapo alitarajiwa kuwa wa kwanza kujitetea.

Kesi hiyo sasa itaendelea tarehe 7 mwezi Aprili.

Oscar Pistorius amekana kumuua mpenziwe Reeva Steenkamp kimaksudi lakini anakiri kufyatua risasi zilizomuua akidai kuwa alidhani ni jambazi aliyekuwa ameingia nyumbani mwake.

Mahakama tayari imesikiza siku 15 za ushahidi kutoka upande wa mashtaka ikiwemo mashahidi waliodai kusikia sauti za kelele na milio ya risasi.

Iwapo atatoa ushahidi ,itakuwa mara ya kwanza kwa bingwa huyo wa mbio za walemavu kuzungumza hadharani kuhusu yaliojiri siku hiyo nyumbani kwake.

Haki miliki ya picha AP
Image caption Kesi ya Pistorius imeahirishwa hadi mwezi ujao

Katika kesi ambayo inafuatiliwa kwa karibu kimataifa Pistorious amekana kumuua mpenzi wake ambaye alikuwa ni mwanamitindo Reeva Steenkamp .

Japo mahakama haiwezi kumlazimisha atoe ushahidi, Pistorious ndiye shahidi pekee katika kesi hiyo ya mauaji na mawakili wake wamekuwa wakiashiria kwamba huenda wakamtaka atoe ushahidi wake moja kwa moja kwanza.

Ushahidi uliotolewa na upande wa mashtaka unaonekana kuegemea dhana kwamba Pistorious ana historia ya matumizi mabaya ya bunduki.