Uturuki yabana mtandao wa YouTube

Serikali ya Uturuki imebana matumizi ya mtandao wa kijamii wa YouTube, siku moja baada ya mahakama kuamuru kusitishwa kwa muda marufuku ya Twitter ambayo waziri mkuu Recep Tayyip Erdogan alitangaza wiki jana.

Duru zinasema kuwa halmashauri ya usimamizi wa teknolojia ya mawasiliano nchini humo, imechukua hatua za kuudhibiti mtandao huo ingawa taarifa tofauti zinasema kuwa mazungumzo yanaendelea ikiwa hatua hiyo ichukuliwe.

Baadhi ya watumiaji wa mtandao huo walishindwa kuutumia kwani ulikuwa umebanwa wakati watu wengine katika sehemu mbali mbali walifanikiwa kuutumia.

Awali, kilichoonekana kama mawasiliano ya siri kati ya maafisa wa serikali hiyo wakizungumzia Syria yalifichuliwa kupitia kwa mtandao huo wa kijamii.

Inaarifiwa mashauriano hayo yaligusia operesheni ya kijeshi dhidi ya Syria na yaliwashirikisha wakuu wa ujasusi , waziri wa mambo ya nje na naibu mkuu wa jeshi wa Uturuki.

Shirika la habari la Reuters linasema kuwa haliwezi kuthibitisha kanda hiyo ingawa inaonekana kuwa taarifa muhimu sana ya serikali ya Uturuki kuwahi kufichuliwa kupitia kwa mtandao wa kijamii.

Bwana Erdogan, atakayeshiriki uchaguzi mkuu siku ya Jumapili, anatuhumu mitandao ya kijami wa kueneza taarifa zisizo za kweli, na alitishia kupiga marufuku YouTube na Facebook.