Mamia wakosa usafiri Kenya.Kunani?

Image caption Ajali nyingi za magari ya umma zinatokea kutokana na uvunjaji mkubwa wa sheria za barabarani

Mamia ya watu mjini Nairobi, Kenya, wamelazimika kutembea kwa miguu kuelekea kazini nchini Kenya huku magari mengi ya uchukuzi wa umma yakizuiwa kuingia barabarani kutokana na kukosa vidhibiti mwendo.

Sheria mpya iliyowekwa mwaka jana inashurutisha magari yote ya usafiri wa umma kuwa na vidhibiti mwendo vya kisasa.

Hii ni sehemu ya juhudi za wizara ya uchukuzi kupunguza ajali za barabarani ambazo zimekithiri nchini humo kutokana na magari kuendeshwa kwa kasi na uvunjaji mkubwa wa sheria za barabarani.

Mengi ya magari ambayo hayako barabarani leo yamekosa kutimiza matakwa mapya ya serikali kwa wahudumu wa sekta ya uchukuzi na usafiri nchini humo.

Wahudumu wa magari ambayo tayari yametekeleza sheria hiyo wamepandisha nauli zao.

Serikali ilikataa kuwaongeza muda wahudumu hao wa kuweza kununua vifaa hivyo hata baada ya muda waliopewa tangu mwezi Disemba mwaka jana kukamilika ikisema kuwa walikuwa wamepewa muda wa kutosha.