WHO kudhibiti Ebola Guinea

Haki miliki ya picha BBC World Service
Image caption Watu 122 wamembukizwa homa hiyo kali kufika sasa Afrika Magharibi

Shirika la afya duniani limesema linachukulia kwa uzito sana mlipuko wa sasa wa homa ya Ebola Magharibi mwa Afrika.

Kufikia sasa shirika la WHO limethibitisha visa 122 vya homa ya Ebola huko Guinea na vingine saba katika nchi jirani ya Liberia.

Hadi sasa watu 80 wamefariki kufuatia maambukizi hayo wengi kutoka Guinea na wanne wakiwa raia wa Liberia.

Huku juhudi zikiendelea kudhibiti homa hii angamizi inayowaua asilimia 95 ya wanaoambukizwa, WHO imeanza kuwachunguza mamia ya raia nchini Guinea.

Shirika hilo limeanza kutuma nguo za kukinga maambukizi pamoja na maafisa wa afya.

Hii ndio mara ya kwanza eneo hilo kushuhudia mulipuko wa homa ya Ebola.

Mara ya kwanza Homa hiyo kuzuka Afrika ilikua mwaka 1976 katika mataifa ya Sudan na iliyokua Zaire kwa sasa Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Huambukizwa kupitia damu na maji ya mwili pia inaweza kuambukizwa kati ya binadamu na wanyama.

Siyo rahisi kutambua Ebola na maafisa wa afya wanaowahudumia wagonjwa wanakumbwa na hatari ya kuambukizwa.Rais wa Guinea amewataka raia kutokua na hofu akisema hatua zote zimechukuliwa kukabiliana na maradhi haya.