Makaburi alizikwa usiku wa manane

Image caption Marehemu Abubakar Shariff Makaburi

Mhubiri mwenye utata aliyeuawa na polisi mjini Mombasa Jumanne usiku, Abubakar Shariff Makaburi alizikwa usiku wa manane kuamkia leo.

Maziko yake yalifanyika saa sita baada ya watu wasiojulikana kumuua akiwa nje ya mahakama ya Shanzu mjini Mombasa.

Makaburi alidaiwa na polisi kuwa mmoja wa watu waliokuwa wanasajili vijana wa kiisilamu kwenda kupigania kundi la wanamgambo wa kiisilamu la Al Shabaab nchini Somalia.

Aliwahi kuhojiwa na BBC na kukiri kuwa yuko tayari kufa kama shahidi wa dini. Makaburi alisema kuwa alijua wazi atauawa hasa baada ya mhubiri mwingine Sheikh Aboud Rogo ambaye alikuwa anaeneza itikadi kali za kiisilamu mjini Mombasa kuuawa.

Makaburi aliuawa akiwa na mhubiri mwingine nje ya mahakama punde tu baada ya kuhudhuria kesi ya washukiwa 29 wa ugaidi mjini Mombasa.

Vijana hao walikuwa miongoni mwa wale waliokamatwa nje ya msikiti Musa kutokana na harakati za polisi kupambana na vijana wanaoeneza itikadi kali za kiisilamu mjini humo mwezi mmoja uliopita.

Duru zinasema kuwa Makaburi alizikwa usiku ili kuzuia vurugu asubuhi yake kutoka kwa vijana waisilamu waliokuwa wameaza kusababisha hali ya taharuki usiku punde baada Marehemu Makaburi aliuawa.