Shambulizi la kujitoa mhanga laua 15

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Watu 15 zaidi wafa Maiduguri

Watu kumi na tano wameuawa na wengine kumi na saba kujeruhiwa katika shambulizi la kujitolea mhanga unaoshukiwa kutekelezwa na kundi la wapiganiji wa kislamu la Boko Haram Nigeria.

Msemaji wa wizara ya ulinzi nchini humo amedhibitisha shambulizi hilo lilifanyika nje ya mji wa Maiduguri katika jimbo la Borno.

Msemaji wa wizara ya ulinzi bwana Chris Olukolade, amesema shambulizo hilo lilitekelezwa na mtu aliyekuwa amebeba vilipuzi katika gari lake.

Mlipuaji huyo wa kujitoa mhanga alijilipua na kusababisha vifo na uharibifu wa magari yaliyokuwa yameegeshwa pahala hapo.

Watu wengine sita walojihusisha na shambulizi hilo waliuawa na vikosi vya usalama, na mmoja kutiwa mbaroni .

Shirka la kutetea haki za kibinadamu la Amnesty International lilisema katika ripoti yake ya hivi punde kuwa watu wasiopungua elfu moja mia tano wameuawa katika mashambulizi kama haya katika

kipindi cha miezi mitatu iliyopita mwaka huu huko Kaskazini mashariki mwa Nigeria.

Shirika hilo limeonya kuwa mashirika ya serikali na wapiganai wa Kiislamu wanakiuka haki za kibinadam.

Shirika hilo limesema kuwa maovu yanayotendwa na kundi hilo lililopigwa marufuku la boko haram yamefikia kiwango cha makosa ya jinai.

Wapiganaji wa Boko Haram wamekuwa wakishambulia raia, wanafunzi idara ya magereza ya Nigeria mbali na kambi za jeshi la taifa .