Mitambo ya analojia yazimwa Tanzania

Tanzania imeingia awamu ya pili ya mpango wake wa mfumo wa matangazo kuhama kutoka analojia kwenda dijitali, kwa kuzima mitambo ya analojia katika baadhi ya miji ya kati na magharibi mwa nchi hiyo.

Miji iliyoingizwa katika mfumo huo kuanzia jumanne wiki hii ni Singida na Tabora wakati ambapo miji mingine saba ikiwemo Kigoma na Kagera itaingizwa kufikia mwezi Mei mwaka huu.

Mkuu wa mawasiliano wa Mamlaka ya mawasiliano Tanzania - TCRA, Inocent Mungy ameiambia BBC mjini Singida kuwa kufikia Novemba 30 mwaka huu watakuwa wamezima mitambo ya analojia katika miji 11 kwa awamu hii ya pili, huku akidai kuwa kazi ya kukamilisha matangazo ya dijitali kwa nchi nzima itakuwa ndani ya muda uliowekwa.

Wakati Tanzania ikiwa mstari wa mbele katika eneo la Afrika Mashariki , Kenya ipo kwenye mgogoro wa kisheria kukamilisha mpango huo.

Kwa mujibu wa mkataba wa kimataifa nchi nyingi duniani zinatakiwa kuhamia matangazo ya digitali ifikapo Juni mwaka 2015.

Je mtango wako umezimwa? Tuma ujumbe wako kwenye ukrasa wetu wa Facebook: https://www.facebook.com/pages/BBC-Swahili/160894643929209