Kiongozi Ubelgiji awasomea Marais wa Afrika

Image caption Waziri mkuu wa Ubelgiji ni kiongozi wa pili Ulaya kutangaza kuwa anashiriki mapenzi ya jinsia moja

Waziri mkuu wa Ubelgiji anayeshiriki mapenzi ya jinsia moja, Elio Di Rupo amewasomea viongozi wa Afrika na kuwataka kuheshimu haki za watu wanaotengwa ikiwemo wapenzi wa jinsia moja.

Alisema ni jambo la kushangaza na lisilokubalika kwamba watu wanahukumiwa kwa sababu ya wanavyochagua kuishi maisha yao.

Bwana Di Rupo alikuwa anahutubia kongamano la viongozi wa Afrika na Muungano wa Ulaya mjini Brussels Ubelgiji lililohudhuriwa na Marais wa Afrika.

Mwaka huu Nigeria na Uganda zilikaza sheria zake kuhusu mapenzi ya jinsia moja.

Nchini Uganda yeyote anayepatikana na hatia ya kushiriki mapenzi ya jinsia moja watafungwa maisha jela

Image caption Wanaharakati wanaopinga mapenzi ya jinsia moja Uganda

Vitendo vya mapenzi ya jinsia moja vimeharamishwa katika nchi nyingi za Afrika ambako mapenzi ya jinsia moja yanaonekana kama kitendo kiovu na kisichokubalika.

Bwana Di Rupo ni afisa wa pili wa ngazi ya juu Ulaya kutangaza kuwa yeye ni shoga. Waziri mkuu wa Ieceland Johanna Sigurdardottir pia amejitangaza kushiriki mapenzi ya jinsia moja.

"hatuwezi kukubali kuwa baadhi yetu wananyimwa haki zao na kuchukuliwa hatua za kisheria kwa kuwa wapenzi wa jinsia moja,'' alisema waziri mkuu huyo

Rais Museveni na mwenzake wa Nigeria Goodluck Jonathan hawajajibu kisomo hicho.

Maafisa wakuu wa Uganda wamekuwa wakitetea msimamo wa Rais Museveni kuhusu sheria yake kali ya mapenzi ya jinsia moja wakisema kuwa Uganda ni nchi huru ambayo mataifa ya magharibi hayawezi kuishawishi hivi hivi.