Mwalimu amuua mwanafunzi Kenya

Image caption Adhabu ya kiboko kwa wanafunzi imeharamishwa katika shule zote nchini Kenya

Wazazi katika kaunti ya Kirinyaga mkoa wa Kati nchini Kenya wameandamana kwa hasira baada ya mwalimu kumchapa mtoto mmoja wa shule ya msingi hadi akafariki.

Mtoto huyo inaarifiwa alichapwa kichwani na mwalimu na kuzirai. Alifariki alipokuwa anapelekwa hospitalini.

Wazazi hao waliandamana kwa amani wakitaka hatua kali kuchukuliwa dhidi ya mwalimu huyo.

Hata hivyo polisi waliweza kumkamata mwalimu huyo na kumpeleka kituoni huku uchunguzi ukianza kufanywa.

Mtoto huyo alikuwa katika darasa la saba katika shule ya kibinafsi ya Roka Preparatory.

Inaarifiwa alizirai baada ya mwalimu kumchapa kwenye kisogo.

Wazazi hao waliokuwa wanalalamikia kile wanachosema ni wanafunzi kuadhibiwa vikali kwa makosa madogomadogo walitaka mwalimu huyo achukuliwa hatua kali kwa kitendo hicho cha kumchapa mwanafunzi ambacho kimeharamishwa katika shule zote nchini Kenya.

Wengi wa wazazi wenye watoto wao katika shule hiyo wameahidi kuwahamishia shule nyingine.

Kenya iliharamisha kitendo cha kuwachapa wanafunzi wa shule karibu miaka kumi iliyopita. Ilikuwa baada ya visa vya walimu kuwaadhibu vikali wanafunzi na kuwajeruhi kukithiri.