Wakimbizi wa Syria, mzigo kwa Lebanon

Image caption Idadi ya wakimbizi hawa Lebanon imefika milioni moja

Idadi ya wakimbizi waliotoroka Syria na kukimbilia Lebanon imeongezeka na kufika watu milioni moja.

Lebanon sasa inasemekana kuwa na idadi kubwa ya wakimbizi Mashariki ya Kati.

Umoja wa Mataifa unasema kuwa kwa nchi kama Lebanon ambayo ina matatizo yake ya ndani , kuwa na wakimbizi wengi kiasi hicho, inaathiri nchi pakubwa.

Takriban watu milioni 9.5 ambao ni takriban nusu ya idadi ya watu nchini Syria, wametoroka nchi hiyo kutokana na vita.

Zaidi ya watu milioni 2.5, wametoroka nchi hiyo wengi wakikimbilia Uturuki,Jordan, Iraq, Misri na nchi nyinginezo katika Mashariki ya kati.

Lakini Lebanon ndio nchi inayokumbwa na matatizo mengi zaidi. Wakimbizi sasa wamefika robo ya idadi ya wenyeji.

Kila mtu anajua idadi kamili ya wakimbizi wa Syria nchini Lebanon imefika watu milioni moja, wengi wamesajiliwa tayari na idadi inatishia kuongezeka.

Lebanon ni nchi ndogo na ambayo inakabiliwa na tisho kubwa kuliko nchi nyingine majirani wa Syria.

Waziri wa mambo ya nje wa nchi hio alisema kuwa huo ni mzigo mkubwa sana kwa Lebanon na unatishia maisha ya watu wa Lebanon.

Umoja wa Matifa umepokea asilimia 14 pekee ya ufadhili unaotakikana . Ina maana kuwa msaada ni mdogo na lazima wanaohitaji zaidi pekee waweze kupewa kipaombele.