Kilimo kufadhili soka Zimbabwe

Image caption Mwenyekiti wa shirikisho la soka Zimbabwe Cuthbert Dube

Mwenyekiti wa shirikisho la soka nchini Zimbabwe, Cuthbert Dube ameelezea kuwa yuko tayari kuendelea na mpango wa kuanza kilimo ili kufadhili soka nchini humo.

Dube alichaguliwa kwa mara ya pili mwishoni mwa wiki na tayari ameiomba serikali kulipa shirikisho hilo mashamba kadha kote nchini ili wafanye kilimo kufadhili shughuli za shirikisho hilo.

Madeni ya shirikisho hilo, yaliongezeka na kufika dola milioni 6 katika muhula wa kwanza wa Dube wa miaka minne na anatafakari zaidi anavyoweza kutafuta ufadhili kusaidia shirikisho hilo Zifa.

"labda watu wengine watauliza ikiwa niko timamu, lakini tutaanza kilimo kwa njia kubwa ili kujifadhili,'' alisema Dube.

''Nishaanza kushauriana na serikali kuhusu mpango huo, hasa kwa sababu tuko na mpango huu maalum wa mageuzi katika sekta ya matumizi ya ardhi.''

Ushindi wake haukufurahikiwa na watu wengi hasa mashabiki wa soka.

Zimbabwe haijang'aa sana katika soka katika kipindi cha miaka minne iliyopita, isipokuwa kumaliza wanne katika kinyang'anyiro cha kombe la Afrika.

Shirikisho hilo limekuwa na wakati mgumu kufadhili soka, vilabu vya wanawake na wanaume.

Huku uchumi wa Zimbabwe ukidorora, imekuwa vigumu kwa mashirikisho ya michezo kupata wafadhili na Dube anahisi kuwa ni wakati wa kujaribu njia nyinginezo za kujipatia pesa.