Kijana auawa katika mzozo wa mapenzi Kenya

Polisi mjini Nairobi wanachunguza kisa cha mwanafunzi mmoja wa kidato cha tatu anayedaiwa kumuua mwenzake kwa kumdunga kisu.

Tukio hilo lilifanyika siku ya Jumatano mtaani Komarock viungani mwa mji wa Nairobi ambapo wawili hao inaarifiwa wlaikuwa wanazozania msichana mmoja mpenzi wa mmoja wa vijana hao.

Maafisa hao wanamtafuta mshukiwa ambaye anadaiwa kumdunga Geoffery Onyango mwenye umri miaka 16 kisu kifuani alipokuwa akirejea nyumbani kutoka shuleni.

Wenzake wanasema kuwa wawili hao walikuwa na ugomvi kati yao kabla Onyango kudungwa kisu.

Hatimaye alikimbizwa hospitalini lakini alifariki akipokea matibabu.

Mkuu wa Polisi mjini Nairobi alisema kuwa bado wanaendelea kumtafuta mshukiwa huyo.