Ukraine: wanaounga Urusi wavamia miji

Image caption Waandamanaji wanaotaka kujiunga na Urusi wamevamia miji Mashariki mwa ukraine

Rais wa Mpito wa Ukraine, Oleksandr Turchynov, ameitisha mkutano wa dharura wa maafisa wake wa usalama baada ya waandamanaji wanaounga mkono Urusi kuvamia na kuingia katika

afisi za Serikali katika miji mitatu Mashariki mwa Ukraine.

Miji ya Donetsk,Kharkiv na luhansk, ndiyo imeshuhudia maandamano makubwa zaidi .

Waandamanaji walikabiliana na maafisa wa polisi na kuziweka bendera za Urusi katika makao makuu ya miji hiyo .

Wanadai wanataka kufanyike kura ya maoni ili na wao wafuate mkondo wa rasi jirani ya Crimea kujitenga na Ukraine .

Serikali ya Kiev imeishtumu Urusi kwa kuchochea ghasia hizo iliipate fursa ya kuivamia Ukraine kijeshi kwa niya ya kuigawanya.

Kaimu waziri wa usalama wa taifa wa Ukraine Arsen Avakov amesema polisi tayari wamewaondoa waandamanaji ambao walikuwa wamepora silaha kutoka kwenye handaki kuu ya jimbo la Kharkiv.

Matukio hayo yamevutia hisia kali kutoka kwa mataifa jirani ,Rais wa jamhuri ya Czech Milos Zeman amesema kuwa vikosi vya NATO vinafaa kujiandaa kuivamia Urusi kwa kuingilia kijeshi mashariki mwa

Ukraine.

Katibu mkuu wa NATO, Anders Fogh Rasmussen, amenukuliwa akiiambia gazeti la The Daily Telegraph kuwa Urusi inajaribu kuibua makanda yenye ushawishi barani Uropa.