Chelsea yaibana Swansea 1-0

Image caption Chelsea 1-0 Swansea

Chelsea ilisalia katika nafasi ya pili katika jedwali la ligi kuu ya Uingereza licha ya kuilaza Swansea bao moja kwa nunge katika mechi ngumu iliyochezwa jumapili.

Mlinzi wa Swansea Chico Flores alionyeshwa kadi za njano mbili na akalazimika kuondoka uwanjani baada ya dakika 16 tu ya kipindi cha kwanza.

Na kama ulifikiri kukosa mchezaji mmoja ilirahisisha mechi kwa Chelsea umenoa.

Vijana wa Jose Mourinho walilazimika kufanya kazi ya ziada ilikupata bao lao la pekee lililofungwa na Demba Ba kunako dakika ya 68 ya kipindi cha pili.

Ba itakumbukwa aliisaidia Chelsea kuilaza Paris-St Germain katika mechi ya kufuzu kwa nusu fainali ya kombe la mabingwa barani Ulaya jumanne iliyopita.

Kutokana na kichapo hicho,Swansea imedorora hadi nafasi ya 15 ya ligi hiyo yenye timu 20.

Kwa upande wao Chelsea wamesalia katika nafasi ya pili wakiwa na alama 75 alama mbili nyuma ya vinara Liverpool waliosajili ushindi mkubwa wa mabao 3-2 dhidi ya wapinzani wao wakuu Manchester City katika mechi iliyochezwa mapema jumapili.

Manchester city sasa iko katika nafasi ya tatu ikiwa na jumla ya alama 70 lakini ikiwa na mechi mbili zaidi za kucheza.

Liverpool imesalia na mechi nne pekee.

Everton imeipiku Arsenal Katika nafasi ya nne ikiwa na alama 66 mbili zaidi ya The Gunners ambao sasa wanajikita katika nafasi ya 5.

Tottenham ni ya sita na alama 60 huku Manchester United wakiwa katika nafasi ya 7 na alama 57.