Wakenya watamba London Marathon

Image caption Bingwa wa London marathon Wilson Kipsang

Mshikilizi wa rekodi ya dunia katika mbio za Marthon Wilson Kipsang alitwaa taji la mwaka huu la mbio za London Marathon alipoandikisha muda bora wa saa mbili dakika nne nukta 27 (2:04:27).

Mkenya mwenza Stanley Biwott alimaliza katika nafasi ya pili akitumia muda wa saa mbili dakika nne nukta 55 ( 2:04:55)

Bingwa mtetezi wa mbio hizo Tsegaye Kebede kutoka Ethiopia alimaliza katika nafasi ya tatu akiwa ametumia muda wa saa mbili dakika sita nukta 30 (2:06:30).

Katika kitengo cha wanawake wakenya walidhibitisha udedea wao walipotwaa nafasi za kwanza mbili.

Bingwa wa dunia Edna Kiplagat ambaye amemaliza katika nafasi ya pili katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita aljifurukuta katika kilomita ya mwisho na kumpiku Florence Kiplagat vilevile kutoka Kenya.

Edna aliukata utepe baada ya kutimuka mbio hizo za kilomita 42 katika barabara za mji wa London akitumia muda wa saa mbili dakika 20 na sekunde 19 (2:20:19).

Bingwa wa dunia wa mbio mbio za kilomita 21 Florence Kiplagat,alimfuata kwa karibu sana akimaliza sekunde tatu tu nyuma yake.

Kiplagat alisajili muda wa saa mbili dakika 20 nukta 22 ( 2:20:22).

Methiopia mshindi wa dunia wa mbio za mita 5000 na mita 10,000 , Tirunesh Dibaba ambaye alikuwa akishiriki katika marathon yake ya kwanza alikamilisha mbio hizo katika nafasi ya tatu .

Dibaba alisajili muda wa saa mbili dakika 20 na sekunde 33 ( 2:20:33).

Image caption Bingwa wa London marathon Edna Kiplagat

Edna ambaye aliweka jina lake katika vitabu vya historia kwa kuwa mwanamke wa kwanza kuwahi kushinda taji la marathon la dunia katika kipindi cha miaka miwili mfululizo aliiambia BBC kuwa alikuwa amechoshwa na nafasi ya pili. ''Mwaka wa 2012 nilimaliza wapili nyuma ya Mary Keitany akisajili muda wa 2:19:50

Mwaka wa 2013 nikashindwa hata baada ya kukimbia nikitumia muda wa (2:21:32) na Rita Jeptoo ,mwaka huu ilikuwa ni zamu yangu kuhakikisha nimeshinda''.

Ilikuwa shangwe na vigelegele kwa washindi wa mbio hizo walipolakiwa na rais wa Kenya Uhuru Kenyatta aliyekuwa London kumpa mkewe motisha katika mbio hizo.

Bi Magret Kenyatta alishiriki mbio hizo katika azimio la kuchangisha fedha za kuimarisha huduma za afya kwa kinamama wajawazito katika maeno ya mashambani nchini kenya

Anakusudia kutoa magari ya huduma ya kwanza katika majimbo yote 47 ya Kenya.

Bi Kenyatta alimaliza mbio hizo baada ya zaidi ya saa saba na kuwa mke wa rais wa kwanza duniani kuwahi kushiriki na kukamilisha mbio za marathon zenye umbali wa kilomita 42.