Balozi wa Jordan atekwa nyara Libya

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Makundi ya wapiganaji ndiyo yamekuwa yakilaumiwa kwa visa vya utekaji nyara mjini Tripoli

Balozi wa Jordan nchini Libya ametekwa nyara mjini Tripoli, katika shambulizi ambalo limemwacha dereva wake na majeraha mabaya.

Maafisa wakuu kutoka wizara ya mambo ya ndani wamethibitisha tukio hilo, wakisema kuwa dereva wake anapokea matibabu.

Ubalozi wa Jordan mjini Tripoli pia umethibitisha taarifa hiyo bila ya kutoa maelezo zaidi.

Libya imekuwa ikizongwa na misukosuko tangu makundi ya wapiganaji kumuondoa mamlakani hayati Muammar Gaddafi mwaka 2011.

Haijulikani nani ametekeleza shambulizi hilo.

Mnamo mwezi Januari, wafanyakazi watano wa ubalozi wa Misri walitekwa nyara mjini Tripoli kwa siku chache kabla ya kuachiliwa huru.

Makundi ya wapiganaji yamekuwa yakilaumiwa kwa kutekeleza visa kadhaa vya utekaji nyara wa maafisa wakuu nchini Libya

Mara kwa mara hulipwa na serikali ili kuwaachilia watu waliotekwa nyara ingawa haijulikani yanaongozwa na nani.