ICC kushurutisha mashahidi kutoa ushahidi

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Naibu Rais William Ruto na Rais Kenyatta wanakabiliwa na tuhuma za kuchochea ghasia za kikabila nchini Kenya

Mahakama ya kimataifa ya jinai ICC, imewashurutisha mashahidi katika kesi dhidi ya naibu rais wa Kenya William Ruto kutoa ushahidi huo.

Mashahidi hao ni baadhi ya wale waliokataa kutoa ushahidi lakini mahakama imesema ni jukumu la Kenya kuhakikisha kuwa mashahidi hao 8 wanafika Hague kutoa ushahidi au watumie njia ya video kutoa ushahidi wao.

Kulingana na mwendesha mkuu wa mashitaka, Fatou Bensouda, mashahidi hao hawataki kutoa ushahidi na pia wamekataa kushirikiana na ICC katika kesi hiyo.

ICC inataka serikali ya Kenya kuwahakikishia usalama wao ili wawe huru kutoa ushahidi wao.

Bwana Ruto anakabiliwa na tuhuma za kuchochea ghasia za kikabila nchini Kenya mwaka 2007 ambazo zilisababisha vifo vya watu 1,200 na maelfu kufurushwa makwao.

Hatua ya mashahidi kukataa kutoa ushahidi wao imeathiri kesi dhidi ya Ruto hasa kwa upande wa mashitaka.

Ruto alifikishwa Hague pamoja na Rais Uhuru Kenyatta wakituhumiwa kuwa viongozi wakuu waliopanga ghasia hizo.

Kenyatta anatarajiwa kuanza kujibu tuhuma dhidi yake , ingawa na yeye pia amekanusha madai yote dhidi yake.

Kesi yake iliahirishwa hadi Oktoba ili kutoa muda kwa upande wa mashitaka kukusanya ushahidi zaidi baada ya mashahidi wawili wakuu kujiondoa kutoka katika kesi hiyo.