Waasi wa Sudan Kusini wakana mauaji

Image caption Waasi wa Sudan Kusini wamekana mauaji ya raia kwa misingi ya ukabila

Waasi nchini Sudan Kusini wamekanusha madai yaliyotolewa na Umoja wa Mataifa kuwa waliwaua watu kwa misingi ya ukabila.

Msemaji wa waasi, Brigedia Lul Ruai Koang, ameambia BBC kuwa wanajeshi wa serikali ndio waliowaua raia walipokuwa wanaondoka mji wa Bentiu uliotekwa wiki jana na waasi wanaomuunga mkono makamu wa zamani wa Rais Riek Machar.

Umoja wa Mataifa katika ripoti yake iliyotolewa Jumatatu, ulisema kuwa takriban watu miambili waliokuwa wamepewa hifadhi msikitini na wengine wengi wakiwa wanahifadhiwa hospitalini na makanisani waliuawa kwa sababu ya kabila lao.

Jeshi la Sudan Kusini linasema kuwa linakabiliana vikali na waasi hao katika majimbo matatu nchini Sudan Kusini.

Zaidi ya watu milioni moja wamelazimika kuondoka makwao tangu mapigano kuanza Disemba mwaka jana.

Mgogoro huo ni kati ya Rais Salva Kir wa kabila la Dinka na Riekl Machar aliyekuwa makamu wa Rais anayetoka kabila la Nuer

Pande zote mbili zinasemekana kufanya mauaji.

Lakini mauaji yaliyofanywa na waasi mjini Bentiu, Bor na Malakal, umewafanya watu kumchukia kiongozi wa waasi Riek Machar.

Mapigano huenda yakaanza tena ingawa pia mazungumzo ya kusitisha vita yanatarajiwa kuanza nchini Ethiopia katika wiki chache zijazo.

Kumekuwa na taarifa za jeshi kuwalenga watu wa kabila la Nuer huku waasi wakiwalenga watu wa jamii ya Dinka.