Jeshi lapambana vikali na waasi Sudan.K

Image caption Waasi nchini Sudan Kusini wamedaiwa kuwaua watu kwa misingi ya ukabila madai ambayo wamekanusha vikali

Vita vikali vimezuka kati ya waasi na wanajeshi nchini Sudan Kusini.

Kwa mujibu wa msemamaji wa jeshi Kanali Phillip Aguer amenukuliwa akisema kuwa vita vimetokea katika sheemu kadhaa za nchi hiyo ikiwemo mjini Bentiu.

Mapigano makali yanaripotiwa kuendelea Kaskazini Mashariki mwa jimbo la Upper Nile na Mashariki mwa jimbo la Jonglei, amesema Philip Aguer.

Awali, waasi hao walikanusha madai ya Umoja wa Mataifa kuwa waliwaua watu kwa misingi ya ukabila na kisha kudhibiti mji wa Bentiu unaozalisha mafuta.

Makubaliano ya kusitisha vita yalifikiwa mwezi Januari ingawa vita havijakoma.

Zaidi ya watu milioni moja wamelazimika kutoroka makwao tangu mapigano kuanza Disemba mwaka 2013.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Athari za vita katika mji wa Bentiu

Mgogoro huu ni kati ya Rais Salva Kiir wa kabila la Dinka na aliyekuwa makamu wake Riek Machar kutoka jamii ya Nuer.

Bwana Aguer alisema kuwa jeshi pia lililazimishwa kuondoa wanajeshi wake kutoka katika jimbo la Mayom, ili kuandaa upya kikosi chake hasa kutokana na mji wa Bentiu kutekwa na waasi.

"Ushindi wa waasi ni wa muda tu , muda ndio mwamuzi mkuu, lazima wataondoka mjini humo, ''Kanali Aguer aliambia BBC.

Lakini alisema kuwa kuna maeneo mengine ambako waasi hao wanaendesha vita.

Wiki moja iliyopita, mji wa Renk Kaskazini mwa jimbo la Upper Nile, ulishambuliwa na waasi wa Rike Machar.