Sudan Kusini:AU kuunga mkono vikwazo

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Vurugu zimesababisha mamilioni kuhama makwao Sudan Kusini

Muungano wa Afrika umesema kuwa utaunga mkono vikwazo dhidi ya viongozi wa Sudan Kusini waliohusika na mauaji ya halaiki mjini Bentiu.

Naibu mwenyekiti wa muungano huo, Erastus Mwencha, ameyasema hayo huku akilaani mauaji hayo ya mamia ya raia kwa msingi ya ukabila.

Ametoa wito kwa pande zote zinazohusika katika mgogoro huo ulioanza Disemba mwaka jana kufikia mwafaka wa kisiasa.

Mwencha pia ametetea Muungano huo dhidi ya tuhuma kuwa umejikokota katika kukabiliana vilivyo na migogoro katika bara la Afrika.

anachama wa baraza la usalama la Umoja wa Mataifa wanatafakari kuwawekea vikwazo wapinzani katika mzozo wa Sudan Kusini.

Akizungumza baada ya baraza hilo lililokuwa na kikao cha kufahamisha kuhusu hali inayozidi kuwa mbaya nchini humo, balozi wa Marekani katika umoja wa mataifa Samantha Power, alisema kuwa jamii ya kimataifa ni sharti ichukue hatua dhidi ya wale wanaowalenga raia na kuharibu mchakato wa kisiasa unaolenga kuleta suluhu katika mzozo huo.

Awali mkuu wa kikosi cha kulinda amani cha umoja wa mataifa alishutumu pande zote katika mzozo wa Sudan Kusini kwa kushindwa kuzuia vurugu zinazoendelea kukithiri nchini humo.

Hervé Ladsous ameliambia Baraza la Usalama kwamba pande zote haziko tayari kufanya mazungumzo ya amani.