Sudan Kusini: Majeshi yasajili watoto

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Navi Pillay, mkuu wa shirika la haki za binadamu la Umoja wa Mataifa

Askari watoto zaidi ya 9,000 wamekuwa wakipigana katika vita vya kikatili vya wenyewe kwa wenyewe nchini Sudan Kusini, amesema Navi Pillay, mkuu wa shirika la haki za binadamu la Umoja wa Mataifa.

Amesema jeshi la nchi hiyo na majeshi ya waasi yaliwasajili watoto kuingia katika vikosi vyao.

Bi Pillay amesema Sudan Kusini imetishiwa na baa la njaa, lakini hapakuwa na "hali ya kujali" kwa upande wa viongozi wake.

Alikuwa akizungumza mwishoni mwa ziara yake nchini Sudan Kusini, ambako mgogoro kati ya serikali na waasi umesababisha watu wapatao milioni moja kukosa makaazi.

Mapigano yalizuka mwezi Desemba kati ya majeshi yanayomtii Rais Salva Kiir na aliyekuwa naibu wake aliyefukuzwa Riek Machar.

Bwana Kiir alimtuhumu Bwana Machar kwa kula njama ya kumpindua.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Askari waasi Sudan Kusini

Alikanusha tuhuma hizo, lakini baadaye aliandaa jeshi la waasi kupigana dhidi ya serikali.

Pande hizo mbili zilijadiliana mkataba wa kusitisha mapigano mwezi Januari na wamerejelea mazungumzo nchini Ethiopia, lakini mapigano yanaendelea.

Navi Pillay alikutana na viongozi wa serrikali na waasi.

Majeshi ya srerikali na waasi wameshutumiwa kwa uhalifu wa kivita.

Bi Pillay amesema mbali na kusajili askari watoto, majeshi ya serikali na waasi yamefanya mashambulio yaliyosababisha vifo vya raia, wakiwemo watoto.

Alikutana na Bwana Kiir na Bwana Machar wakati wa ziara yake nchini Sudan Kusini na kwa sasa anatarajiwa kwenda Ethiopia.