Kikosi cha EU chadhibiti ulinzi CAR

Image caption Wanajeshi wa EU watakuwa chini ya kamanda wa majeshi ya Ufaransa ambao tayari wako nchini humo

Wanajeshi wa Muungano wa Ulaya wamedhibiti ulinzi katika uwanja rasmi wa ndege katika Jamhuri ya Afrika ya Kati

Hii ndio operesheni ya kwanza kubwa nchini CAR tangu wanajeshi 150 kupelekwa mnini Bangui katika wiki chache zilizopita baada ya taarifa kuibuka kuwa kuna tisho la mauaji ya kimbari.

Karibu robo ya watu milioni 4.6 wa nchi hiyo wametoroka makwao tangu kuzuka vita tarehe 13 mwezi Machi kati ya wapiganaji waisilamu na wakristo.

Muungano wa Afrika ukishirikiana na serikali ya Ufaransa, ulipeleka wanajeshi 7,000 nchini humo.

Wamekuwa wakipambana vilivyo dhidi ya wapiganaji ili kusitisha mgogoro unaokumba nchi hiyo, na sasa muungano wa Ulaya umeahidi kupeleka wanajeshi 1000 huku Umoja wa Mataifa ukipeleka wanajeshi 12,000.

Mji wa Bangui umeshuhudia vita vibaya sana na ni wiki jana tu wanajeshi wa AU walipowasindikiza zaidi ya waisilamu 1,200 kwenda nchi jirani huku wakitoroka vita hivyo.

Wanajeshi wa EU wako chini ya kamanda wa jeshi la Ufaransa, Meja Generali Philippe Ponties.

Kupelekwa kwao katika uwanja wa ndege , ni moja ya njia za kuwawezesha wanajeshi wa Ufaransa kwenda kwingineko nchini humo ambako wapiganaji wapo.

Haki miliki ya picha
Image caption Waisilamu bado wanatoroka Bangui kutokana na vita

Maafisa wa Umoja wa Mataifa na mashirika ya misaada yameonya kuwa uhasama kati ya wakristo na waisilamu huenda ukasababisha mauaji ya kimbari na hata kugawanya nchi.

Waisilamu wachache bado wako mjini Bangui , wengi wao wametorokea katika nchi jirani.

Wakristo ndio wengi nchini CAR na kundi la wapiganaji wa kikristo la anti-balaka linasema kuwa lilianza mapigano baada ya kushambuliwa na wapiganaji wa Seleka ambao ni waisilamu mwezi Machi mwaka jana.

Kiongozi wa Seleka, Michel Djotodia alilazimika kuondoka mamlakani kwani hali nchini CAR ilikuwa inaendelea kuwa mbaya.

Alikuwa rais wa kwanza Muisilamu. Wafuasi wake wanatuhumu wanajeshi wanaomuunga mkono Rais aliyeng'olewa mamlakani Francois Bozize, kwa kuchochea ghasia.