Milipuko miwili yatikisa Mombasa, Kentya

Image caption Watu 3 wamefariki ingawa idadi hiyo huenda ikaongezeka

Watu 4 wameripotiwa kufariki katika milipuko miwili iliyotokea eneo la Katikati mwa Mombasa pwani ya Kenya.

Mashambulizi haya yametokea wakati polisi nchini humo wakiendelea kufanya misako kwa lengo la kudhibiti usalama.

Mlipuko wa kwanza ulitokea ndani ya basi ya usafiri na kuharibu vibaya basi pamoja na kusababisha hali ya taharuki miongoni mwa wasafiri waliokuwa wanajitayarisha kwa safari zao.

Mlipuko wenyewe ulitokea katika kituo cha mabasi cha Mwembe Tayari. Watu watatu walifariki papo hapo.

Mlipuko huo pia uliharibu basi nyingine iliyokuwa karibu na basi ya kwanza iliyolipuliwa.

Inaarifiwa watu kadhaa wamejeruhiwa katika mashambulizi hayo.

Mlipuko wa pili ulitokea katika hoteli ya Reef ingawa hakuna majeruhi walioripotiwa katika mlipuko huo.

Mashambulizi haya yanakuja wakati hali ya usalama imedbitiwa nchini kutokana na harakati za wanamgambo wa Al Shabaab nchini humo ambao tayari wameshambulia baadhi ya maeneo ya nchi hiyo.

Polisi pia wanasema kumekuwa na ongezeko la vijana wa kiisilamu kufuata itikadi kali za kiisilamu na kushirikiana na kundi la Al Shabaab.

Hakuna aliyekiri kufanya mashambulizi hayo. Kenya imeshuhudia mashambulizi ya kigaidi ya mara kwa mara mjini Mombasa pamoja na mjini Nairobi.

Wakazi wa Mombasa wamekuwa wakilalamika kwa kusema kuwa eneo hilo limetengwa na serikali na sasa mji huo unageuka na kuwa kitovu cha harakati za vijana wa kiisilamu wanaoonekana kuunga mkono harakati za kundi la wanamgambo la Al Shabaab.