Boko Haram kuwauza wasichana waliotekwa

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Kiongozi wa Boko Haram Abubakar Shekau

Kundi la wapiganaji wa kiislamu nchini Nigeria la Boko Haram limesema linapanga kuwauza wasichana zaidi ya miambili ambao liliwateka nyara wiki tatu zilizopita

Hii ni baada ya kundi hilo hatimaye kukiri ndilo lililowateka wasichana hao baada ya kimya cha wiki tatu tangu kutekwa nyara kwao.

Kiongozi wa kundi hilo, Abubakar Shekau alituma kanda ya video ambapo alikiri kwa mara ya kwanza kuwa kundi hilo ndilo liliwateka nyara wasichana hoa.

Wasichana hao walitekwa kutoka shule moja iliyo kaskazini mashariki mwa nchi walipokuwa wajinadaa kwa mitihani yao.

Wakati huo huo mwanamke ambaye ni kiongozi wa maandamano ya kushinikiza serikali kuharakisha juhudi zake za kuwaokoa wasichana hao, nchini humo Naomi Mutah aliyekuwa amezuiliwa na polisi kwa amri ya mke wa rais wa nchi hiyo Patience Jonathan ameachiwa huru.

Kumekuwa na shinikizo kwa serikali ya nchi hiyo kwamba haijafanya juhudi kubwa kuwaokoa wasichana hao.

Akizungumza kwa mara ya kwanza kuhusu tukio hilo rais wa Nigeria Goodluk Jonathan amesema kuwa atafanya awezalo kuwakoa wasichana hao.

Takriban watu 1500 wameuawa na kundi hilo mwaka huu likisema kuwa linapigana dhidi ya kile linachosema ni elimu ya kimagharabi.