Stuart Hall akiri kumdhalilisha msichana

Haki miliki ya picha
Image caption Stuart Hall, mtangazaji wa zamani wa BBC

Mtangazaji wa zamani wa BBC, Stuart Hall amekiri kumdhalilisha kimapenzi mtoto wa kike chini ya umri wa miaka 16 lakini amekana mashitaka mengine 20 yanayomkabili.

Bwana Hall, mwenye umri wa miaka 84, ataendelea na kesi akituhumiwa makosa 15 ya ubakaji na mengine matano ya udhalilishaji dhidi ya wasichana wawili akituhumiwa kuyatenda kati ya mwaka 1976 na 1981 katika miji ya Greater Manchester na Cheshire.

Kosa la nyongeza ambalo amekiri limemfikisha mbele ya mahakama ya Preston Crown Court.

Mahakama imeambiwa kuwa shambulio hilo la aibu lilifanyika kati ya mwezi Januari 1978 na Januari 1979.

Bwana Hall, kutoka Wilmslow, Cheshire, anakabiliwa na mashitaka saba ya ubakaji dhidi ya msichana mmoja kati ya mwaka 1976 na 1978, huko Manchester.

Makosa matano ya ubakaji yanasemekana kufanyika dhidi ya msichana huyo akiwa na umri wa miaka chini ya 16.

Pia anatuhumiwa kutenda makosa mawili ya shambulio la aibu dhidi ya msichana huyo katika kipindi hicho hicho.

Zaidi ya hapo, ameshitakiwa kwa makosa nane ya ubakaji na matatu ya udhalilishaji dhidi ya msichana mwingine kati ya mwaka 1976 na 1981, katika maeneo tofauti katika miji ya Greater Manchester na Cheshire.

Moja ya makosa ya ubakaji anayotuhumiwa kutenda Bwana Hall, inasemekana kufanyika wakati mlalamikaji alipokuwa na umri chini ya miaka 13.