Mashahidi zaidi kumtetea Oscar Pistorius

Haki miliki ya picha AP
Image caption Oscar Pistorius akikabiliwa na kesi ya mauaji ya mpenzi wake Reeva Steenkamp nchini Afrika Kusini

Jopo la utetezi katika kesi ya mauaji inayomkabili mwanariadha wa Afrika Kusini, Oscar Pistorius limeitisha mashahidi zaidi, wakati huu wakitaka kuthibitisha kuwa Pistorius alimuua mpenzi wake Reeva Steenkamp bila kukusudia.

Majirani wa karibu kabisa na Bwana Pistorius wamesema Jumanne kuwa walisikia mtu akilia kwa nguvu usiku wa mauaji hayo.

Jumatatu watu wengine wawili- ambao walikuwa wa kwanza kufika eneo la tukio- walielezea juhudi alizokuwa akifanya kuokoa maisha ya Bi Steenkamp.

Mwanariadha huyo anatuhumiwa kumuua Bi Steenkamp siku ya Valentine, mwaka jana.

Pistorius amekana tuhuma za kumuua makusudi mpenzi wake na anasema alimpiga risasi kupitia mlango wa chooni akiwa ametaharuki, akidhani mtu aliyekuwa anamshambulia ni mwizi aliyeingia nyumbani mwake.