Jokofu kuwasaidia maskini Saudi Arabia

Image caption Baadhi wametoa wito kwa jamii kuiga mfano huu mzuri wa kuwasaidia masikini

Mwanamume mmoja mjini Hail, nchini Saudi Aarabia amejitolea na kuweka Jokofu nje ya nyumba yake na kutoa wito kwa majirani kulijaza na vyakula ili kuwasaidia maskini.

Gazeti la Gulf News linaripoti kuwa, mwanamume huyo ambaye hakutaka kujulikana aliwaambia majirani wake kuwa jambo hili litawaondolea maskini aibu ya kuomba chakula.

Habari hizi zilichipuza baada ya mhubiri mmoja maarufu wa Kiislamu kusifu hatua hio kwenye mtandao wa twitter. Sheikh Mohamad al-Arefe aliandika kuwa ‘nimekuwa nikisema watu wa Hail ni wakarimu.

''Mwanamume mmoja ameweka jokofu nje ya nyumba yake ili kuweka mabaki ya chakula: njia ya kuonyesha upendo na kutoa msaada kwa maskini . Oh, jinsi ninavyoipenda Hail.’ Kauli hiii ya sheikh Mohamad ilisambazwa zaidi ya mara 5000, kwa mujibu wa mtandao wa habari wa Akhbar.

Watumiaji wa mitandao ya kijamii wanatoa wito kwa misikiti na nyumba zingine kuweka nje majokofu kama hatua ya kuonyesha ukarimu kwa jamii.

Mtu mwingine naye akiongeza sauti yake, amesema kuwa watu wapaswa kuweka chakula ambacho kimepikwa na si mabaki tu.

Aliongeza kusema kuwa ni jambo la kulisha sio mwili tu bali hata nafsi kupitia vitendo vikuu vya upendo na msaada kwa maskini hasa kwa muda unaoelekea mwezi mtukufu wa Ramadhan, utakaoanza rasmi mwishoni mwa mwezi Juni.