Sudan.K :Mahasimu wakutana ana kwa ana

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Waasi wa Sudan Kusini wamekuwa wakizozana na wanajeshi wa serikali tangu mwaka jana

Mazungumzo ya kutafuta amani sudan Kusini yanaendelea hivi sasa mjini Addis ababa Ethiopia ambapo rais wa Sudan Kusini Salva Kiir amewasili tayari kukutana na mpinzani wake na kiongozi wa waasi Riek Machar.

Hii ndiyo mara ya kwanza kwa viongozi hao mahasimu kukutana ana kwa ana tangu mapigano kuzuka mwezi Disemba mwaka uliopita .

Rais Salva Kiir alimfuta kazi makamu wake Riek Machar na kuibua mgawanyiko uliotibua vita baina ya wafuasi wao katika jeshi Desemba tarehe 15.

Machar ameonya kuwa mazungumzo hayatapiga hatua iwapo majeshi ya serikali yatakuwa yakiendelea na uvamizi wao katika maeno yanayodhibitiwa na wafuasi wa waasi.

Maelfu ya watu wameuawa huku zaidi ya watu milioni moja kulazimika kutoroka makwao kuepuka vita .

Ripoti moja ya umoja wa mataifa imezilaumu pande zote husika kwa kutekeleza mauaji ya halaiki na kukiuka haki za binadamu.

Marekani inasema kuwa haina matumaini kuwa mazungumzo ya leo yataweza kuleta mafanikio yoyote.

Mgogoro huo wa kisiasa umesababisha maelfu ya watu kufariki huku zaidi ya wengine milioni moja wakiachwa bila makao.

Katika ripoti yake hapo jana, Umoja wa Matifa ulituhumu pande zinazozana kwa kufanya vitendo vya kukiuka haki za binadamu ikiwemo mauaji, ubakaji, kuwafanya wanawake kuwa watumwa wa ngono, kufanya mauaji ya halaiki na kuwabaka wanawake,.

Ripoti hiyo ilisema kuwa vitendo vingi vya uhalifu vilifanywa katika nyumba za watu, hospitali, misikiti , makanisani na katika makao ya umoja wa Mataifa ambako wakimbizi walikuwa wamekimbilia usalama wao.

Image caption Umoja wa Mataifa umetuhumu upande wa Rais Kiir na ule wa Machar kwa kukiuka haki za binadamu

Kadhalika ripoti hiyo imesema kuwa takriban watu milioni 5 wanahitaji msaada wa kibinadamu.

Mkataba wa amani ulifikiwa kati ya Rais Kiir na Machar mnamo mwezi Januari lakini haukusitisha mapigano.

Wapatanishi nchini Ethiopia, wamethibitisha kuwa bwana Machar aliwasili Alhamisi kwa mazungumzo hayo mjini Addis Ababa.

Mazungumzo ya leo yatalenga kumaliza vita na kusuluhisha tatizo la kugawana mamlaka.

Mawaziri wa serikali wamesema kuwa kile ambacho serikali inakipa kipaombele ni kusitisha vita na kujadili swala la kipindi cha mpito.

Hata hivyo, Waziri wa mambo ya nje Barnaba Marial Benjamin, alinukuliwa akisema kuwa swala la serikali ya mpito halitajadiliwa na kuwa Rais Kiir ataendelea kuwa Rais hadi uchaguzi mwingine utakapofanyika mwaka 2015.