Mkalimani wa mazishi ya Mandela aajiriwa

Image caption Mkalimani aliyekashifiwa Thamsanga Jantjie

Je unamkumbuka mkalimani huyu aliyeuduwaza ulimwengu kwa utafsiri wake wa ishara wakati wa mazishi ya hayati mzee Nelson Mandela mwaka uliopita ?

Thamsanqa Jantjie aliyekashifiwa na ulimwengu mzima na haswa walemavu kwa kutoa ishara zisizotafsirika kwa wale wenye matatizo ya kusikia wakati wa mazishi ya aliyekuwa rais wa Afrika Kusini Nelson Mandela sasa amepata ajira . Jantjie alijitetea kuwa alishikwa na kiwewe na kuona mazingaombwe wakati wa maziko hayo.

Haki miliki ya picha AP
Image caption Mkalimani aliyekashifiwa Thamsanga Jantjie karibu na rais Obama

Bwana huyo sasa ameonekana katika tangazo la biashara akikejeli tukio hilo lililompa umaarufu kote duniani.

Tangazo hilo la linapigia debe mtandao wa kijamii wa Livelens uliotengezwa na kampuni moja kutoka Tel Aviv Israili.

Afisa mkuu mtendaji wa kampuni hiyo Max Bluvbland ameiambia BBC kuwa Jantjie yuko timamu na kuwa alitekeleza majukumu yake bila tashwishi yeyote ''yeye ni mtu timamu aliyepatikana na mkasa anaojutia.

Wataalamu wa lugha za ishara walisema mtafsiri huyo wa lugha za ishara, alikuwa "akitapatapa" wakati wa ibada hiyo.

Naibu Waziri wa Afrika Kusini Hendrietta Bogopane - Zulu alikanusha kuwa kulikuwa na suala la kukiuka taratibu za kiusalama wakati mtafsiri huyo alionekana akisimama kwenye jukwaa wakati wa ibada hiyo iliyokuwa ikitizamwa kote duniani na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali.